Gibraltar imepinga ombi la Marekani kuikamata tena meli ya mafuta ya Iran ambayo ilikuwa ikiizuia tangu mwezi Julai kwa kudhania kwamba ilikuwa ikisafirisha mafuta Syria.
Marekani iliwasilisha ombi la mwisho siku ya Ijumaa , siku moja baada ya Giraltar kuiachilia meli hiyo ya Grace 1.
Gibraltar imesema kwamba haikuweza kukubali ombi la Marekani kuikamata tena meli hiyo kwa kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran havina nguvu Ulaya.
Meli hiyo tayari imeondoka Gibraltar kulingana na mjumbe wa Iran nchini Uingereza.
Tehran imesema kwamba iko tayari kuyapeleka majeshi yake kuisindikiza meli hiyo ambayo jina lalke lilibadilishwa kutoka Grace 1 hadi Adrian Drya 1.
Meli hiyo na wafanyakazi wake 29 kutoka India, Urusi, Latvia na Ufilipino ilikamatwa kupitia usaidizi wa wanamaji wa Uingereza tarehe 4 Julai baada ya serikali ya Gibraltar - eneo linalomilikiwa na Uingereza kusema kwamba ilikuwa ikielekea Syria hatua inayokiuka vikwazo vya Muungano wa Ulaya.
Hatua hiyo ilizua mgogoro wa kidiplomasia kati ya Uingereza na Iran , ambao umeendelea katika wiki za hivi karibuni huku Iran nayo ikiikamata meli iliokuwa ikipeperusha bendera ya Uingereza Stena Impero katika Ghuba.
Mamlaka ya Gibraltar iliiwachilia meli hiyo siku ya Alhamisi baada ya kupokea hakikisho kutoka Iran kwamba haitaipeleka mafuta yake nchini Syria.
Idara ya haki nchini Marekani baadaye ikawasilisha ombi mahakamani la kuizuilia meli hiyo kwa msingi kwamba ina uhusiano na jeshi la Iran ambalo imelitaja kuwa kundi la kigaidi.
Gibraltar , katika taarifa yake siku ya Jumapili ilisema kwamba haikuweza kukubali ombi hilo kwa kuwa jeshi hilo la Revolutionary Guard sio kundi la kigaidi kulingana na EU ambalo eneo hilo la Uingereza ni mshirika wake.
Pia ilisema kwamba vikwazo vya Marekani vya kuzuia uuzaji wa mafiuta wa Iran haviwezi kuidhinishwa na EU ikidai tofauti iliopo kati ya Marekani na EU kuhusu Iran.
Hakujakuwa na majibu yoyote kutoka kwa Washington.
Balozi wa Iran nchini Uingereza Hamid Baedinejad alituma ujumbe wa twitter siku ya Jumapili kwamba makundi mawili ya wahandisi wa Iran walikuwa wanaelekea Gibraltar na kusema kwamba meli hiyo inatarajiwa kuondoka usiku.
Stena Impero, ambayo ilikamatwa na jeshi la Revolutionary Guard tarehe 19 Julai bado ipo mikononi mwa Iran.
Uingereza imetangaza kwamba itajiunga na kundi la wanajeshi wa Marekani kulinda meli za biashara zinazosafiri kupitia mkondo wa Hormuz.
Meli iliokuwa ikipeperusha bendera ya Uingereza Stena Impero ilikamatwa na Iran tarehe 22 Julai
Hali ya wasiwasi kati ya Iran na mataifa ya magharibi inatokana na mpango wa kinyuklia wa Iran.
Mwaka uliopita, Washington ilijiondoa katika mkataba wa kinyuklia wa Iran wa 2015 ili kuzuia taifa hilo kutengeza silaha za kinyuklia huku kukiwa na wasiwasi kwamba Tehran ilikuwa inajaribu kuunda silaha za kinyuklia , kitu ambacho Iran imekana.
Tangu wakati huo , wasiwasi kati ya Marekani na Iran umeongezeka huku taifa hilo likiiongezea vikwazo Iran.
Uingereza na mataifa mengine ya Ulaya yamesema kwamba bado yanaheshimu mkataba huo.